Idadi ya waliofariki Nepal yafikia 1,287, huku 5,083 hawajulikani walipo
Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la Nepal linalosimamia majanga limesema miili ya watu 1,287 imepatikana hadi sasa, huku ikikadiriwa kuwa watu 5,083 bado hawajulikani walipo.
Hili ni ongezeko kutoka kwa takwimu za awali zilizotolewa na polisi nchini humo, ambazo zilisema watu 1,280 walikuwa wamefariki na 4,798 walikuwa hawajulikani walipo.
Watu wawili wameokolewa wakiwa hai kutoka katika eneo lililoporomoka katika mradi wa kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji wa Trishuli 3A nchini Nepal, siku tisa baada ya mafuriko makubwa kuikumba nchi hiyo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200.
Timu za uokoaji bado zinaendelea na juhudi za kuwaokoa watu wengine wanaodaiwa kunaswa ndani ya eneo hilo.
Suresh Raut, afisa mwandamizi wa Mamlaka ya Umeme Nepal ambaye yuko katika eneo la uokoaji, ameiambia BBC kuwa waokoaji walikuwa wakimpatia oksijeni mmoja wa watu waliookolewa, ambaye mamlaka zimemtambua kwa jina la Sanjaya Shah.
Marekani yachunguza shambulio la kombora kwenye harusi nchini Iran
Chanzo cha picha, Iranian Red Crescent Society
Jeshi la Marekani linafanya uchunguzi kuhusu madai ya Iran kwamba shambulio la kombora nchini humo liliwaua watu wasiopungua wanne, wakiwemo watoto wawili, katika hafla ya harusi kusini mwa Iran, kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance.
Shirika la Hilali Nyekundu la Iran (IRCS), linalotoa msaada wa kibinadamu, limesema roketi ilipiga hafla ya harusi iliyokuwa ikifanyika katika nyumba moja mjini Sirik siku ya Jumanne.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, alielezea tukio hilo kuwa ni “uhalifu wa kivita.”
Makombora ya Marekani yalirushwa siku hiyo hiyo baada ya Iran kujaribu kushambulia vikosi vya Marekani.
Hata hivyo, msemaji wa Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) alisema vikosi vya Marekani “kamwe havilengi raia.”
Akizungumza Alhamisi, Vance alisema alikuwa “na mashaka makubwa” kuhusu taarifa za shambulio hilo linalodaiwa, lakini alithibitisha kuwa Marekani ingefanya uchunguzi.
“Naweza kusema kwamba vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali ya Iran havijawa chanzo kizuri cha taarifa kuhusu kinachoendelea katika mzozo huu hadi sasa. Kwa hiyo, nina mashaka makubwa kuhusu hili,” Vance alisema katika mkutano na waandishi wa habari Ikulu ya White House.
“Ninatambua kuwa tunafanya uchunguzi.” Iran imeanzisha mashambulizi mapya dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani nchini Kuwait na Falme za Kiarabu (UAE), ikiwa ni kulipiza kisasi dhidi ya shambulio hilo linalodaiwa.
Maduro, mkewe waomba kuondolewa mashtaka ya usafirishaji wa dawa za kulevya
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa zamani wa Venezuela Nicolás Maduro na mkewe Cilia Flores, wameiomba mahakama ya Marekani kufuta mashtaka ya usafirishaji wa dawa za kulevya yanayowakabili.
Katika nyaraka zilizowasilishwa katika mahakama ya shirikisho ya Manhattan Jumatano, mawakili wao wamedai kuwa wana kinga dhidi ya mashtaka hayo kwa sababu Maduro alikuwa rais na Flores alikuwa mke wa rais.
Mawakili wa Maduro wamesema sheria za kimataifa haziruhusu mahakama za nchi moja kumfungulia mashtaka kiongozi wa nchi nyingine.
Flores anadai kuwa kinga hiyo inatokana na uhuru wa Venezuela na kwamba ni nchi hiyo pekee inayoweza kuiondoa.
Maduro na Flores wamekana mashtaka hayo.
Waendesha mashtaka wa Marekani wanasema Maduro na Flores walihusika katika mpango wa kusafirisha kwa magendo maelfu ya tani za kokeini kwenda Marekani, kwa kushirikiana na vikosi vya usalama vya Venezuela.
Iwapo watapatikana na hatia kwa makosa hayo, wanaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.Wawili hao wamezuiliwa Brooklyn tangu walipotekwa na vikosi vya Marekani katika operesheni iliyofanyika Caracas, Januari 1, 2026.
Marekani ilisema operesheni hiyo ilikuwa halali, lakini Maduro amesema hakuridhishwa nayo.Jaji Alvin Hellerstein atasikiliza hoja za pande zote mnamo Novemba 17. Kesi kuu imepangwa kuanza Juni 1, 2027, iwapo ombi lao litakataliwa.
Umoja wa Mataifa wasema wapiganaji wa kigeni wanachochea vita nchini Sudan
Chanzo cha picha, Reuters
Umoja wa Mataifa unasema wapiganaji wa kigeni, silaha na teknolojia ya kijeshi kutoka nje zinaendelea kuchochea vita nchini Sudan, huku nchi kama Somalia zikitajwa katika mtandao unaodaiwa kusaidia pande zinazopigana.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaochunguza ukweli kuhusu mzozo huo umesema msaada huo umeongeza uwezo wa jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kufanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo ya raia yaliyo mbali na uwanja wa vita.
Vita vilianza Aprili 2023 kutokana na mzozo wa kugombea madaraka kati ya jeshi na RSF, na hadi sasa vimewalazimisha zaidi ya watu milioni 14 kuyahama makazi yao.
Ripoti hiyo imesema zaidi ya watu 1,000 waliuawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika miezi mitano ya kwanza ya 2026, huku pande zote mbili zikishutumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu.
Umoja wa Mataifa unasema baadhi ya vitendo hivyo vinaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita.
Wachunguzi pia wanaamini kuwa mtandao unaohusisha watu na taasisi katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Chad, Libya na Somalia umeipa RSF silaha, vifaa, msaada wa vifaa na usafirishaji, mafunzo pamoja na wapiganaji wa kigeni.
Umoja wa Mataifa pia unasema hadi wakandarasi 2,000 kutoka Colombia walisaidia kuendesha na kutunza mifumo ya ndege zisizo na rubani na silaha nyingine za kisasa zinazotumiwa na RSF.
Baadhi yao walikuwepo wakati wa operesheni karibu na Al-Fashir, Darfur, mji ambao RSF iliuteka Oktoba 2025.
Umoja wa Mataifa umesema mauaji yaliyofanyika huko yalikuwa na viashiria vya mauaji ya kimbari.
UAE imekanusha mara kwa mara kutoa msaada wa kijeshi kwa RSF, huku Colombia ikisema inapinga shughuli za mamluki na imechukua hatua kukabiliana na ushiriki wa raia wake katika migogoro ya nje.
Somalia imesema inachukulia kwa uzito tuhuma hizo, na kwamba haitaruhusu ardhi, anga au bandari zake kutumiwa kwa madhumuni ya kijeshi na pande zinazohusika katika vita vya Sudan.
Hata hivyo, serikali hiyo imekiri kuwepo kwa mapengo katika ushirikishwaji wa taarifa kati ya serikali ya shirikisho na tawala za kikanda.
Chad, kupitia balozi wake mjini Geneva, imekanusha tuhuma hizo na kusisitiza kuwa haina upande wowote katika mzozo huo.
Katika kile kinachoelezwa kama vita vya ndege zisizo na rubani, Umoja wa Mataifa unasema silaha hizo zilizoingizwa kutoka nje zimeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa jeshi la Sudan na RSF kufanya mashambulizi ya masafa marefu.
Waziri wa Fedha wa Marekani: Umoja wa Ulaya umejiunga na operesheni ya kuitenga Iran kiuchumi
Chanzo cha picha, EPA
Waziri wa
Fedha wa Marekani, Scott Besant, akirejelea taarifa ya mawaziri wa fedha na
magavana wa benki kuu wa kundi la G20, alitangaza kuwa "Umoja wa Ulaya
umejiunga rasmi na 'operesheni ya kuitenga Iran kiuchumi'" na kwamba
Marekani "inathamini msimamo wao thabiti na wa mapema."
Bw. Besant
aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X: "Marekani inasimama kidete
pamoja na washirika wetu kuhakikisha kuwa utawala wa uhalifu wa Iran hauwezi
kutumia mfumo wa kifedha wa kimataifa kufadhili malengo yake ya nyuklia,
programu za silaha, na makundi ya kigaidi yanayofanya kazi kwa niaba
yake."
Waziri wa
Fedha wa Marekani amesisitiza kuwa "dunia inatoa ujumbe wa wazi kwa
utawala wa Iran: 'Hatutaacha hadi njia ya mwisho ya uhai wa kifedha
itakapokatwa.'"
Siku mbili
zilizopita, Tume ya Ulaya ilitoa taarifa pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa
fedha na magavana wa benki kuu wa G20 huko Asheville, ikiunga mkono vikwazo vya
Marekani dhidi ya Iran.
Figo ya nguruwe iliyopandikizwa kwa binadamu yafanya kazi kwa siku 271
Chanzo cha picha, Kate Flock/Massachusetts General Hospital
Figo
iliyopandikizwa kutoka kwa nguruwe imefanya kazi mwilini mwa mgonjwa kwa siku
271 – muda mrefu zaidi kuwahi kurekodiwa, kulingana na madaktari nchini
Marekani.
Tim Andrews
amesema upandikizaji huo ulimpa "matumaini" na kumwepusha na miezi
kadhaa ya kulazimika kwenda hospitalini ili damu yake isafishwe kwa mashine.
Timu ya
wataalamu katika hospitali ya Mass General Brigham inasema kazi yao inaonyesha
kuwa viungo vya nguruwe vinaweza kutumika kama "daraja" la muda hadi
pale kiungo cha binadamu kitakapopatikana kwa ajili ya upandikizaji.
Hata hivyo,
kiungo hicho cha nguruwe hatimaye kilishindwa kufanya kazi na kikaondolewa,
hivyo Andrews alihitaji kufanyiwa dayalisisi kwa muda mfupi kabla ya kupatikana
kwa mtoaji.
Madaktari na
wanasayansi wanachunguza uwezekano wa kupandikiza viungo kutoka kwa viumbe wa
spishi nyingine – kutokana na uhaba wa viungo kwa ajili ya upandikizaji.
Nchini
Marekani, takriban watu 100,000 wanasubiri figo, huku upandikizaji wa figo
25,000 pekee ukifanyika kila mwaka.
Nchini
Uingereza, zaidi ya watu 7,000 wako kwenye orodha ya wanaosubiri kupandikizwa
figo.
Andrews
aliambiwa kuwa inaweza kuchukua miaka saba kufikia orodha hiyo, ilhali kwa wastani watu huishi
miaka mitano tu wakiwa wanategemea matibabu ya dayalisisi.
DR Congo yaahhidi kuhamisha ubalozi wake wa Israel mjini Jerusalem
Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo imetangaza siku ya Alhamisi kuwa itahamishia ubalozi wake
nchini Israel hadi Jerusalem, ikijiunga na kundi dogo la nchi, ikiwemo Marekani,
katika kuchukua hatua hiyo yenye uzito wa kidiplomasia ya kuunga mkono mamlaka
ya Israel juu ya mji huo mtakatifu wenye utata.
Kufuatia
ziara ya Rais Felix-Antoine Tshisekedi, nchi hizo mbili zilisema katika taarifa
kuwa zitachukua hatua za "kuhamisha ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem", bila kutaja muda maalum wa
kufanyika kwa hatua hiyo.
Taarifa hiyo
ilieleza kuwa, katika mkutano wao, Tshisekedi na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin
Netanyahu walizungumzia "nia yao ya pamoja ya kuimarisha uhusiano wa
kidiplomasia".
Waziri Mkuu nchini
Israel Benjamin Netanyahu amesema siku ya Alhamisi kuwa kuuangusha utawala wa
Jamhuri ya Kiislamu ni jambo "linalowezekana kufikiwa," akisisitiza
kuwa utawala huo ni dhaifu kuliko wakati wowote ule na unapambana ili kusalia
madarakani.
Katika hafla
iliyohusisha viongozi wa kijeshi, aliongeza kuwa anaamini inawezekana
"kuondoa" kabisa tishio la Iran, akilitaja hilo kuwa ndilo jukumu kuu
linaloikabili Israel bado.
Netanyahu amesema
kuwa hatua ya Iran kutolenga Israel katika mzunguko wa hivi karibuni wa
mashambulizi haikuwa bahati mbaya, akiongeza kuwa Tehran inafahamu vyema nguvu,
silaha, na azimio la Israel.
Netanyahu
anajiandaa kushiriki katika uchaguzi wa bunge wenye ushindani mkali mwishoni
mwa mwezi wa Oktoba.
Waziri wa
Ulinzi wa Israel, Yisrael Katz, alisema nchi yake iko tayari kujibu "kwa
nguvu kubwa" iwapo Iran itashambulia wakati wa sikukuu za Kiyahudi, zinazoanza
katikati ya mwezi wa Septemba, akibainisha kuwa Iran ililenga maeneo mbalimbali
katika eneo hilo, isipokuwa Israel, wakati wa mzozo huo wa hivi karibuni.
Mamlaka na wakaazi wapambana kuzima moto Mlima Kilimanjaro
Chanzo cha picha, Jackson Mauki
Mamlaka na
wakazi wa kaskazini mwa Tanzania wanapambana kuzima moto unaowaka kwenye
miteremko ya Mlima Kilimanjaro, ambao ni mlima mrefu zaidi barani Afrika.
Moto huo
unateketeza eneo lililoko katika mwinuko wa takriban mita elfu tatu na mia nne
juu ya usawa wa bahari.
Afisa wa
Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania ameiambia BBC kwamba bado haijafahamika
kilichosababisha moto huo kuwaka.
Mlima
Kilimanjaro, ambao ni muhimu kwa bioanuwai na utalii, umekumbwa na visa vingine
vikubwa vya moto wa nyika viliyosababisha uharibifu katika miaka ya hivi
karibuni.
Mwaka 2023,
moto uliodumu kwa takriban wiki moja uliharibu eneo la kilomita 17 za mraba,
sawa na takriban asilimia moja ya eneo la hifadhi ya mlima huo.
Korea Kusini inajitayarisha kutuma askari kwenye Mlango Bahari wa Hormuz
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Korea Kusini
Vyombo vya
habari vya Korea Kusini vimeripoti kwamba serikali ya nchi hiyo inajiandaa
kupeleka vifaa na vikosi vya kijeshi ili kuunga mkono kile kinachoitwa
"uhuru wa urambazaji katika Mlango-Bahari wa Hormuz" na inapanga
kuanza misheni hii kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Reuters
iliandika Alhamisi (Septemba 3) kwamba ripoti katika vyombo vya habari vya
Korea Kusini, zikinukuu vyanzo vya serikali na kijeshi, zilisema Seoul
inachukua hatua muhimu za kisheria ili kupata idhini ya bunge kwa ajili ya
kupelekwa huko.
Kulingana na
ripoti hizi, baada ya kukagua mpango huo katika Baraza la Mawaziri, serikali
inapanga kuwasilisha ombi rasmi la idhini ya bunge mwezi huu.
Uwezekano wa
kupelekwa kwa vikosi vya Korea Kusini unakuja huku mvutano wa usalama katika
Mlango-Bahari wa Hormuz na mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara
yakiongezeka katika wiki za hivi karibuni, na nchi kadhaa zinachunguza njia za
kushiriki katika kulinda usalama wa meli katika njia hii ya kimkakati ya maji.
Maafisa wa
serikali ya Korea Kusini bado hawajajibu rasmi ripoti hizi.
Shambulio baya dhidi ya sherehe ya harusi nchini Iran huenda lilisababishwa na kombora la Marekani - Reuters
Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la
habari la Reuters liliripoti katika taarifa ya kipekee kwamba, kulingana na
uchambuzi wa wataalamu wa silaha waliochunguza picha na video zilizothibitishwa
na shirika hilo, mlipuko uliolenga sherehe ya harusi katika mji wa Kohstak
kusini mwa Iran siku ya Jumanne, ambao uliua watu watano na kujeruhi angalau 68,
una uwezekano mkubwa wa kusababishwa na shambulio la moja kwa moja la silaha ya
Marekani, badala ya athari isiyo ya moja kwa moja au kuruka kwa silaha hiyo
baada ya kugonga lengo jingine.
Katika
ripoti hiyo iliyochapishwa Alhamisi, Septemba 3, Reuters iliandika:
"Reuters iliwasilisha picha na video za shambulio hilo kwa wataalamu wanne
wa silaha.
Wataalamu
hao walisema kuwa namna uharibifu ulivyotokea inaashiria shambulio la moja kwa
moja la silaha moja, na si mlipuko uliosababishwa na silaha hiyo kuruka
kwingine baada ya kugonga lengo jingine."
Watatu kati
ya wataalamu hao pia waliambia Reuters kwamba "ushahidi uliopo unaonyesha
kuwa silaha hizo zina uwezekano mkubwa wa kuwa zimetengenezwa Marekani, na si
kombora la ulinzi wa anga la Iran lililopotea njia."
Gareth
Collet, brigedia jenerali mstaafu wa Jeshi la Uingereza na mtaalamu wa kutegua
mabomu mwenye shahada ya uzamivu katika uhandisi wa vilipuzi, aliambia Reuters
kuwa inawezekana silaha hizo zilikosa tu lengo lake lililokusudiwa.
Reuters
inasema afisa wa Marekani, aliyeomba kutotajwa jina, alithibitisha kuwa
Marekani ilifanya shambulio la anga katika eneo la Kohstak usiku wa Jumanne, kwa
lengo la kuharibu vifaa vya kijeshi vya IRGC.